WAKULIMA WATAKIWA KUJIFUNZA KILIMO HIFADHI KUPITIA VIKUNDI



















Ni mchana, jua likiangaza katika shamba la Martin Sawema jijini Mwanza karibu na ziwa Victoria kaskazini mwa Tanzania. Bw. Sawema ni kijana wa miaka 31 mhitimu wa chuo kikuu akiwa na stashahada, anafanya kazi mjini kama mwana habari. Pia analima matama na ufuta wilayani Rorya.

Kama ilivyo kwa wakulima wengine, Bw. Sawema anakumbana na vikwazo mbalimbali. Anaeleza, “Ukosefu wa mvua na mbolea na kukosa jenereta la kupandisha maji kwaajili ya umwagiliaji inaathiri mavuno yangu.”

Kutafuta msaada, Bw. Sawema na baathi ya wakulima kijijini kwao wameunda kikundi kiitwacho Kilimo ni Pesa. Wataalamu wa kilimo wa kata na vijiji siku zote hawapatikani, na wakati mwingine inawalazimu wakulima kulipa ili kupata huduma. Lakini wakulima wanapojiunga katika vikundi ni rahisi kwa afisa ugani kusafiri na kuenda kuwapatia huduma.

Bw. Sawema anashauku kubwa kufanya kilimo hifathi, lakini hakujua wapi pa kuanzia. Lakini baada ya kujifunza kupitia kikundi cha Kilimo Ni Pesa, aliacha kuchoma masalia ya mabaki ya mmea baada ya kuvuna na kufanya kilimo hifathi.

Dominick Ndentabura ni mtaalamu wa kilimo wilayani Rorya. Anasema wakulima wanapojiunga katika vikundi, ni rahisi kuwapa mafunzo na ushauri.

Richard Nguvava ni mkurugenzi wa umoja wa Mtandao wa Wakulima Nyancha (Nyancha Farmers’ Network) au MVIWANYA, amboyo inajiendesha kama shrikila lenye vikundi vidogovidogo ndani mwake, ikiwemo kikundi cha Kilimo Ni Pesa. Anasema kabla wakulima hawajaunda vikundi, ilikuwa ngumu kwao kupata ushauri kutoka kwa maafisa ugani.

Bw. Nguvava anaongeza: “Vikundi vya wakulima ni vya muhimu sana kwasababu kupitia vikundi hivi wakulima wanaweza kubadilishana taarifa, wakulima wanabadilishana taarifa kuhusu kilimo cha kisasa na taarifa za masoko, na kuwa wakulima wabunifu. Kwa mfano, [baathi ya vikundi] wameanzisha kilimo hifathi kutunza mazingira.”

Anasema kilimo hifathi kinasaidia kutunza afya ya udongo kwa kuboresha umbile la udongo na kukinga thidi ya mmomonyoko na kupoteza rutuba. Namna mbili ambazo wakulima wanaweza kufanya hivi ni kwa kufunika udongo na kuepuka kusumbua udongo. Kitendo hiki kinaongeza kuwepo kwa rutuba.

Baathi ya wakulima, kama Bw. Sawema, wanatumia mabaki ya mazao kufunika ardhi kuliko kuyafukia ardhini. Au wanatengeneza mboji au kupanda mazao funika. Hii inasaidia kufanya udongo kuwa na rutuba kwa muda mrefu.

Witness Elias ni mama wa watoto watatu anayeishi kijiji cha Bukama katika wilaya ya Rorya. Ni mwanachama wa kikundi cha Tuinuane, kikundi cha wakulima ambacho wana shirikishana taarifa za mbinu bora za kilimo kama kilimo hifathi.

Bi. Elias amenufaika kwa kufanya kilimo hifathi, kilimo ambacho amejifunza katika kikundi chake. Anaelezea, “Nimeona maendeleo mengi. Sasa ninaweza kulipa ada [ya watoto wangu] wanaosoma sekondari na ninampango wa kujenga nyumba ya kisasa.”

Anasema afya ya udongo wake imebadilika baada ya kuanza kufanya kilimo hifathi. Kipindi cha nyuma alikuwa akichoma mabaki ya mimea na kupanda aina moja mazao mika na miaka. Baada ya kujifunza kuhusu kilimo hifathi kupitia kikundi chake cha kilimo, alianza kufanya kilimo mzunguko na kutumia masalia ya mazao kufunika ardhi.

Hii imemsaidia kuongeza mavuno yake. Anasema: “Kabla … nimepata mifuko mitatu tu ya mahindi … lakini sasa ninajivunia mavuno yangu yameongezeka kufikia magunia 10 mpaka magunia 15 ya mahindi katika hekari moja.”

Bi. Elias ni rahisi kwake kupata huduma za mtaalamu wa kilimo akiwa katika kikundi chake cha kilimo kuliko kumlipa mtu binafsi.

Bw. Sawema, akifanya kazi na wakulima wengine katika kikundi imemsaidia yeye kuongeza mavuno yake. Alitumia kipato cha ziada kumalizia ujenzi wa nyumba ya Mama yake. Sasa hategemei moja kwa moja mshahara wake kusaidia familia yake.

Mwaka jana, alivuna gunia 10 za mtama na gunia 5 za ufuta. Alipata shilingi milioni moja na laki tano 1,500,000 (kama dola 650). Kukabiliana na mvua chache, anajipanga kununua jenereta kusaidia kumwagilia shamba lake.

Bw. Sawema anasema anapenda kilimo na anaamani kuwa ndoto zake za kumiliki shamba zimetimia.

Kazi hii imeandaliwa na msaada kutoka Canadian Foodgrains Bank kama sehemu ya mradi, “Kilimo hifathi kwa ustahimilivu, kilimo bunifu kinachoendana na mabadiliko ya hali ya nchi.” Kazi hii imewezeshwa na mfuko wa serikali ya Canada, kupitia Global Affairs Canada, www.international.gc.ca.




No comments