NG'OMBE 341,098 WAPIGWA CHAPA SIMANJIRO


Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti (wapili kulia) baada ya kupewa zawadi ya nguo ya jadi na wafugaji wa kata ya Naisinyai kwenye ziara yake Wilayani Simanjiro, kulia ni Mkuu wa wilaya hiyo mhandisi Zephania Chaula na kushoto ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Jackson Leskar Sipitieck na Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa huo Arnold Msuya. 


Ng'ombe 341,098 wamepigwa chapa Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, ili kutekeleza agizo la Serikali la upigaji chapa mifugo kwa ajili ya utambuzi na kuepuka migogoro ya mara kwa mara. 

Katibu Tawala wa Wilaya ya Simanjiro Zuwena Omary, aliyasema hayo juzi wakati akisoma taarifa kwa mkuu wa mkoa huo Alexander Mnyeti. Omary alisema lengo la wilaya hiyo ni kupiga chapa ng'ombe 437,925 hivyo wamefikia asilimia 79 hadi kufikia Desemba 31 mwaka jana. 
Alisema zoezi hilo lilitarajiwa kukamilika mwezi Desemba mwaka jana ila baada ya serikali kuongeza muda hadi Januari 31 mwaka huu, watakuwa wamefanikiwa kukamilisha. Alisema wilaya hiyo ina mabwawa mawili ya Nyumba ya Mungu na Kidapash, ambayo shughuli za uvuvi zinafanyika na jitihada za kudhibiti uvuvi haramu zimefanyika. 
Kwenye sekta ya kilimo, umwagiliaji na ushirika alisema kuna ekari 346,000 zinazofaa kwa kilimo ambapo takribani ekari 144,00 hutumika kwa kilimo cha mazao ya chakula na biashara. "Mahitaji ya chakula kwa mwaka kwa wakazi wote ni tani 42,000 za nafaka na hali ya chakula ni ya kuridhisha kwenye maeneo mengi kwani wananchi wanatumia chakula kilichovunwa msimu wa Kilimo wa 2016/2017. 
Alisema kwa upande wa mradi wa maji kutoka mto Ruvu hadi mji mdogo wa Orkesumet, serikali itautekeleza kupitia sh40 bilioni, za fedha za ndani na ufadhili wa benki ya maendeleo ya watu wa uarabuni. Mkuu wa mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti aliagiza kila wilaya ya mkoa huo kuhakikisha inakuwa na viwanda 15 ili kutekeleza agizo la serikali la kila mkoa uwe na viwanda 100.

Mnyeti alisema wilaya ya Simanjiro iwe na viwanda 15 na nyingine zitekeleze hilo ili kuhakikisha uzalishaji wa ajira unafanyika na kufikia lengo la kuwa na uchumi wa kati.

Post a Comment

0 Comments