EKARI 130,000 ZA MITI KUTUNZA NA KUPANDWA NA WAKAZI WA UYUI
HALMASHAURI ya Wilaya ya Tabora imeagiza kila kaya katika eneo hilo kuhakikisha inapanda miti ekari moja na kutunza miti asili ekari moja ikiwa ni mpango wake wa kuhakikisha zoezi la uhifadhi wa mazingira na upandaji wa miti linakuwa endelevu.
Kauli hiyo ilitolewa jana katika Kijiji cha Mbuyuni Kata na Kigwa na Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Said Ntahoondi wakati aliposhiriki zoezi la wiki ya upandaji miti kwa upande wa Mashirika yasiyokuwa ya Kiserikali(NGO,s) mkoani Tabora.
Alisema kuwa kwa kutumia idadi ya kaya 65,000 zilizopo katika Halmashauri hiyo watapanda jumla ya ekari 130,000 za miti asili na ile ya kupanda.Ntahondi alisema lengo ni kuzifanya kila kaya kuwa kuwa na mistu yao kwa ajili ya kuwajengea utamaduni wa uhifadhi wa mazingira na upandaji wa miti endelevu kwa ajili yao na nchi kwa ujumla.
Mwenyekiti huyo wa Halmashauri ya Wilaya ya Tabora aliongeza kuwa mpango mwingine wanaoendelea nao ni pamoja na kuhakikisha kuwa kila kaya inapanda miti mitano ya matunda tofauti katika eneo la nyumba yao.
Alisema kuwa hatua itawawezesha kupanda miti ya matunda 325,000 katika kaya zote 65,000 zilizopo katika Halmashauri hiyo.Ntahondi alisema kuwa miche hiyo ya matunda ni nje ya ile iliyopandwa kwa mujibu wa makubaliano na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kuhakikisha kuwa wanapanda matunda mahuleni, hospitalini, Maofisini na barabarani.
Alisema lengo ni kutaka kuwa na matunda mengi kwa ajili ya matumizi ya familia na ya ziada kwa ajili ya uuzaji.
Post a Comment