MPINA APANGUA HOJA ZA WABUNGE KUHUSU NAMNA WIZARA YAKE INAVYOPAMBANA KUTOKOMEZA UVUVI HARAMU NCHINI


Mwenyekiti wa Kamati iliyoundwa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Luhaga Mpina, Injinia Arcard Mutalemwa (Mwenye shati jeupe), kufanya tathmini ili kujua uwekezaji uliopo katika Ranchi za Taifa (NARCO) akikabidhi ripoti ya kazi hiyo jana kwa Waziri Mpina na viongozi wakuu wa Wizara hiyo. Mhe. 
Picha ya pamoja baina ya Kamati iliyoundwa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Luhaga Mpina (mwenye suti nyeusi na miwani) kufanya tathmini ili kujua uwekezaji uliopo katika Ranchi za Taifa (NARCO) kushoto kwake ni Injinia Arcard Mutalemwa, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dkt. Maria Mashingo Katibu Mkuu wa Mifugo, kulia ni Naibu Waziri Abdalah Ulega na Mtendaji Mkuu wa NARCO,Profesa Philemoni Wambura
Mwenyekiti wa Kamati iliyoundwa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Luhaga Mpina, Injinia Arcard Mutalemwa (aliyesimama), kufanya tathmini ili kujua uwekezaji uliopo katika Ranchi za Taifa (NARCO) akisoma na kuwasilisha ripoti ya kazi hiyo jana kwa Waziri Mpina na Viongozi wakuu wa Wizara hiyo.
Mtendaji Mkuu wa NARCO,Profesa Philemoni Wambura akichangia hoja kwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Luhaga Mpina, kwenye kikao cha kukabidhi taarifa ya kamati ya kufanya tathmini ya uwekezaji uliopo katika Ranchi za Taifa (NARCO) jana.



WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina amepangua hoja zilizotolewa na wabunge kuhusu namna Wizara yake inavyopambana kutokomeza uvuvi haramu ili kunusuru kupotea kabisa kwa samaki na kuchochea kufa kwa viwanda vya samaki na kusababisha kupungua kwa ajira nchini.
Waziri Mpina alitoa ufafanuzi huo wakati akijibu hoja za baadhi ya wabunge bungeni Mjini Dodoma ambao walikosoa hatua zinazochukuliwa na Wizara hiyo katika kupambana na uvuvi haramu hususan katika Ziwa Victoria pamoja na kudhitibi utoroshaji wa samaki na mazao yake nje ya nchi.
“Mimi na Wizara yangu tutahakikisha hili tunalisimamia kwa nguvu zote, hizi ni rasilimali za taifa na haziwezi kugawanwa kwa ukanda, rasilimali hizi zinapashwa kunufaisha nchi nzima kwa hiyo kama Wizara inayosimamia Sheria zilizopitishwa na Bunge hili tutahakikisha kwamba hakuna kabisa uvuvi haramu katika nchi yetu, hakuna mfanyabishara atakayejihusisha na kuuza wala kusambaza nyavu haramu, hakuna kiwanda kitakachochakata samaki wasioruhusiwa, hakuna mtu yoyote atakayevua kwa vyavu haramu wala kufanya biashara haramu ya mazao ya uvuvi ni lazima mali zetu tuzilinde kwa nguvu zote” alisisitiza.
Akifafanua hoja hiyo alisema Wizara yake katika kupambana na suala la uvuvi haramu na utoroshaji wa mazao ya uvuvi inatumia Sheria ya Uvuvi namba 22 ya Mwaka 2003 pamoja na kanuni zake za mwaka 2009, Sheria ya Uvuvi wa Bahari Kuu ya Mwaka 1998, na marekebisho yake ya mwaka 2007,Sheria ya Mazingira namba 20 ya Mwaka 2004, Sheria ya Uhujumu Uchumi (Economic and organized crime Act Cap 200 CE 2002 as amended by Act no 3 of 2016) na Sheria ya Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu namba 29 ya mwaka 1994. 
Wabunge hao waliokuwa wakichangia taarifa ya Kamati ya Kilimo, Mifugo na Maji ni pamoja na Joseph Msukuma wa Geita Vijijini, Constantine Kanyasu na Geita mjini na Dk Raphael Chegeni wa Busega
Mpina alisema kwa mujibu wa tafiti zilizofanywa na Wizara yake samaki aina ya Sangara wanaoruhusiwa kuvuliwa wenye urefu wa kati ya sentimita 50 mpaka 85 wamebaki asilimia 3 samaki wazazi wamebaki asilimia 0.4 samaki wachanga wasioruhusiwa kuvuliwa chini ya sentimita 50 ni asilimia 96.6 kwa mantiki hiyo hatuna samaki wanaofaa kuvuliwa katika Ziwa Victoria.
Alisema Kamati hiyo imezungumzia juu ya viwanda vya samaki kufungwa ambapo kabla uvuvi haramu haujashamiri kulikuwa na viwanda 13 vilivyokuwa na uwezo wa kuchakata tani 1, 065 na kutoa ajira 4,000 katika ukanda wa Ziwa Victoria lakini kutokana na kuendelea na uvuvi haramu vimepungua na kubaki 8 vyenye uwezo wa kuzalisha tani 171 na kusababisha kubaki na ajira 2,000 tu.
Mpina aliongeza kuwa Kamati ya Bunge imetoa msukumo mkubwa kwa Wizara hiyo kupitia katika ukurasa wa 32 wa taarifa yao kwamba Serikali iongeze bidii katika kupambana na uvuvi haramu sambamba na kuhakikisha wale wanaotorosha samaki na mazao yake wanawadhibitiwa vilivyo.
Aidha, Mpina alisema katika operesheni hiyo, maamuzi hayafanywi na mtu mmoja katika kutafsiri mambo mbalimbali ikiwa ya vipimo vya nyavu za ngazi mbili au tatu badala yake timu nzima ya wataalamu inachambua na kuishauri Serikali hatua zinazopaswa kuchukuliwa.
Aliongeza kwamba Kamati hiyo imejuisha Maafisa Uvuvi, Maafisa kutoka Baraza la Mazingira la Taifa(NEMC), Jeshi la Polisi,Ofisi ya Rais, Tamisemi, Idara ya Uvuvi .

“Lakini mheshimiwa Mwenyekiti mambo tuliyoyaona kwenye operesheni hii yanatisha zipo gari za waheshimiwa wabunge tumezikamata na samaki haramu,wapo wenyeviti wa halmashauri ,wapo wenyeviti wa vijiji, madiwani, watendaji wa Serikali tumewasimamisha kazi kwa hiyo katika operesheni hiyo tulipokagua viwanda tukakuta viwanda vyote vinachata samaki wasioruhusiwa, tumekamata viwanda vya nyavu haramu”alisema.
Aidha baadhi ya Wabunge akiwemo Mbunge wa Kishapu, Suleiman Nchambi na Mbunge wa Kigoma Mjini, Peter Serukamba kwa nyakati tofauti walimtaka Waziri Mpina kutaja hadharani majina ya wabunge hao wanaotuhumiwa kufadhili uvuvi haramu. 
“ Waziri amesema katika shughuli hii ya kutokomeza uvuvi haramu kuna magari ya wabunge yamekamatwa na samaki ambao wamevuliwa kiharamu,kuna wenyeviti wa halmashauri ambao magari yao yamekamatwa na samaki ambao wamevuliwa kiharamu hawa watu ni wabaya wanaangamiza Taifa letu nakuomba mheshimiwa Waziri uwataje watu hawa ili tuwalaani” alisema Serukamba.
Aidha Waziri Mpina alisema kwa sasa timu yake inakamilisha taarifa ya awamu ya kwanza ya operesheni Sangara mwaka 2018 inayoendelea ambayo iko mbioni kumaliza na kwamba ataifikisha mbele ya kamati na baadae taarifa hiyo itaingia bungeni.
Kufuatia mjadala huo,Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Azzan Zungu aliwataka wabunge kuacha kumpa taarifa Waziri Mpina kwani tayari ameshaeleza kuwa taarifa ikikamilika ataiwasilisha kwenye kamati. 
“Waziri ameeleza vizuri ,tuhuma za watu amezitaja taarifa inaandaliwa itawasilishwa kwenye muda muafaka end of the story sasa ninyi mnakataa nini hatupigi daku hapa kuanzia sasa hakuna taarifa yoyote mhe Waziri maliza..”alisema Zungu.
Aidha Waziri Mpina alisema Serikali imekamata zaidi ya kilo 133,000 ya samaki aina ya kayabo na dagaa zikitoroshwa kwenda Rwanda, Burundi, Kongo na Kenya, pia wamekamatwa samaki wachanga kilo 73,000 ambazo rasilimali hizi zote za nchi zinachezewa kwa kiasi huku operesheni hiyo ikiwakamata hadi raia wa kigeni kutoka Rwanda, Kenya na Burundi wakiwa ndani ya visiwa wakishiriki uvuvi na kununua samaki jambo ambalo ni kinyume cha sheria.
Pia walikamata viwanda vya mabondo 22 vinafanya biashara lakini vilivyokuwa na leseni halali ni viwili tu hivyo Serikali ikisema inapambana na uvuvi haramu inapambana kweli kweli huku akisisitiza kuwa operesheni hiyo haina mwisho hadi uvuvi haramu utakapomaliza hapa nchini
Kuhusu Uvuvi wa Bahari Kuu Waziri Mpina alisema tayari Serikali imeshapata meli ya kufanya doria kwani ilizoeleka meli hizo zinakuja kuvua na kuondoka huku taifa letu linaachwa halina chochote.
“Tunashindwa kukusanya chochote na ndio maana kwa mara ya kwanza tumekamata meli na kuipiga faini milioni 770 nilitegemea Bunge hili litapongeza jitihada hizi kubwa za Wizara ambazo zinalinda rasilimali hizi leo hii mkakati wa kulinda uvuvi wa bahari kuu tutazikagua meli zote zikiwa zinavua huko huko hakuna mtu atakayeondoka kwenye maji ya Tanzania akiwa amebeba rasilimali za watanzania”alisema. 
Alisema Serikali itaongeza meli mbili za doria katika ili kuhakikisha uvuvi wa bahari kuu pamoja na bahari nzima unalindwa kwa nguvu zote na kuhakikisha kwamba rasilimali nchini mwetu zinanufaisha Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Hataruhusiwa mtu yoyote na niseme Mheshimiwa Mwenyekiti kama mtu atajishughulisha na uvuvi haramu aache mimi Mpina hata Mzee Mpina mwenyewe ninyi doria mkamateni kama anajishughulisha na uvuvi haramu hatuwezi kuongelea kwa maneno mepesi mambo makubwa ya mstakabali wa taifa letu’alisema.
Waziri Mpina alisisitiza timu yake ya doria kufanya kazi kwa weredi kwa kufuata sheria na kutokumwonea mtu yeyote wakati wa operesheni hii. Aidha alisema katika ulinzi wa rasilimali za taifa Serikali ni walinzi tu hivyo mlinzi ukikutwa mlango wa tajiri umevunjwa atakuwa na shida .
“Mimi ni kibarua wenu kazi yangu ni kuhakikisha katika wizara mliyonipa rasilimali zinalindwa kwa nguvu zote na kazi hiyo mimi na wizara yangu tutaifanya usiku na mchana lakini nasema kama kuna hoja ya msingi wabunge wasituhumu kwa ujumla yawezekana kuna mtendaji akakosea katika kuchukua hatua, unasema katika eneo fulani katika kijiji fulani kuna jambo hili na hili limefanyika Mpina lishughulikie hata sasa hivi ukiniletea nitafanyia kazi na kuchukua hatua mara moja ”alisema.
Alisema rasilimali za taifa zimetoroshwa vya kutosha na kwamba Bunge muda wote limekuwa likilia juu ya makusanyo hafifu yatokanayo na uvuvi ambapo Serikali inakusanya wastani wa bilioni 20 tu ukiwaondoa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) hivyo ni wakati sasa wa Bunge kuisaidia Wizara kuinua sekta hiyo .
Kuhusu Ranchi za Taifa (NARCO) Waziri Mpina alisema Kamati ilishauri Serikali ifanye tathmini ili kujua uwekezaji uliopo katika ranchi hizo unatija ili ije na mapendekezo sahihi ya namna bora ya kuwekeza katika ranchi hizo ambapo alisema tayari Wizara imeshaunda kamati hiyo inayoongozwa na Afisa Mtendaji Mkuu Mstaafu wa DAWASA, Arcard Mutalemwa.

No comments