WAKULIMA WA PAMBA KANDA YA ZIWA WANOLEWA

Wakala wa Vipimo Tanzania (WMA) chini ya usimamizi wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji imeendelea kutoa elimu  kwa wakulima  pamoja na kuhakiki mizani itakayotumika kununulia zao la Pamba ikiwa ni maandalizi ya msimu wa ununuzi wa Pamba kwa mwaka huu (2018).  Zoezi hili la utoaji elimu na uhakiki wa mizani itakayotumika kununulia Pamba  linaendelea  katika Mikoa ya Shinyanga, Geita, Simiyu, Mwanza, Tabora, Mara pamoja  na Kagera kwa kushirikiana na Ofisi ya Wakala wa Vipimo Makao Makuu.

Dhumuni kuu  la utoaji elimu  kwa wakulima wa zao la Pamba  Kanda  ya Ziwa  ni kuwawezesha  wakulima  kutambua mizani iliyosahihi   (inayoruhusiwa kwa biashara)  na ile iliyochezewa (isiyoruhusiwa kwa biashara)  ili waweze kujilinda wenyewe pindi maafisa vipimo wanapokuwa hawapo katika vituo vya kuuzia Pamba yao na pia ni kuwawezesha wakulima kupata  faida ya thamani kamili ya jasho lao.  
 Meneja wa Wakala wa Vipimo Mkoani Mwanza, Hemed Kipengere akitoa elimu kwa wakulima wa Pamba Wilayani Magu kuhusiana na mambo muhimu ya kuzingatia kabla ya kupima Pamba kwenye mizani ili Wakulima waweze kupata faida ya jasho lao la kulima Pamba.

Akizungumza na  Meneja Sehemu ya Elimu, Habari na Mawasiliano Bi. Irene John,  alisema katika maandalizi ya msimu mpya wa ununuzi wa Pamba Mwanza wanategemea kutoa elimu kwa Wilaya tano (5), Simiyu  Wilaya tano (5), Shinyanga Wilaya tatu (3), Geita wilaya sita (6), Tabora   Wilaya tatu (3) , Kagera Wilaya mbili (2) pamoja na Mara Wilaya tano (5). Hivyo, kwa mwaka huu jumla ya Wilaya 28 zimelima Pamba na zote zitapatiwa elimu  inayohusu matumizi ya vipimo sahihi  na faida zinazopatikana kwa mkulima kwa kuuza mazao yake kupitia mizani iliyohakikiwa na Wakala wa Vipimo.

Mwaka huu tofauti kidogo na mwaka jana maana Serikali imefufua Vyama vya Ushirika ambapo ununuzi wote wa Pamba utafanywa na Vyama vya Msingi  ambayo vinasimamiwa na wakulima wenyewe badala ya kuuza Pamba yao kupitia Mawakala kama ilivyokuwa imezoeleka miaka ya nyuma.  Mkulima wa Pamba atanufaika zaidi  kwa kuuza mazao yake kupitia vyama vya msingi sababu mazao yote  yatakayopatikana  kutoka kwenye Pamba yaani mbegu pamoja na nyuzi  mkulima atahusika kupata faida ya uuzaji wa mazao hayo tofauti na mwanzo faida kama hii ilikuwa haipatikani kwake isipokuwa kwa mfanyabiashara tu.
 Afisa wa Wakala wa Vipimo mkoani Mara wakionesha mizani sahihi na ile isiyo sahihi ili wakulima waweze kujilinda wenyewe pindi maafisa wanapokuwa hawapo.

Pia kuuza Pamba kupitia vyama vya msingi itapunguza ulaghai kwenye mizani sababu wasimamizi na watumiaji wa Mizani watakuwa ni  wakulima wenyewe wa Pamba wala siyo mawakala.
 Irene  alisema Sheria ya Vipimo Sura 340 inawataka Wakala wa Vipimo  kuhakiki na kupiga chapa vipimo vyote vinavyotumika katika biashara ikiwa ni pamoja na  kuweka   sticker kwa kipimo kitakachokuwa tayari kimehakikiwa na kukutwa kikiwa sahihi  ili iwe rahisi kwa wakulima kuona na kutambua mizani iliyokaguliwa na kuruhusiwa kwa biashara kwa mwaka husika.

Bi. Irene ameongezea kuwa Wakala wa Vipimo itaendelea kufanya ukaguzi wa kushtukiza  na wakawaida wakati wowote  baada ya msimu wa ununuzi wa Pamba kuanza ili panapokuwa na malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu uonevu katika mizani yaweze kutatuliwa kwa haraka.
 Bi. Irene John  aliwasihi wakulima wanaolalamikiwa kuweka maji, kokoto pamoja na mchanga kwenye Pamba kwa ajili ya kuongeza uzito waache tabia hiyo mara moja  ili kuleta biashara ya haki.
 Lengo kuu la Wakala wa Vipimo ni kumlinda mlaji ili apate faida na thamani ya kile alichozalisha  na siyo kupunjwa  na wafanyabiashara  wajanjawajanja.  Irene  alisisitiza kuwa kwa wale watakaobainika kuchezea mizani  kwa ajili ya kuwaibia wakulima  adhabu imeboreshwa kuanzia mwaka juzi ( Nov. 2016) hivyo, faini  itaanzia  laki moja  badala ya elfu kumi kama ilivyokuwa imezoeleka kufikia  hadi milioni ishirini endapo mkosaji atakubali kosa.  Kesi ikifikishwa mahakamani na mlalamikiwa akakutwa kweli alikosa kulingana na ushahidi utakaokuwa umetolewa mshitakiwa atatozwa faini kuanzia laki tatu hadi milioni hamsini au kifungo cha miaka mitatu au vyote kwa pamoja.

Irene alisema Tanzania ya viwanda itafanikiwa  endapo Mkulima, Mfanyabiashara watazingatia matumizi ya vipimo sahihi kuanzia maandalizi ya shamba, upandaji wa mazao, utumiaji wa pembejeo, uuzaji, usafarishaji, upokeaji wa mazao, ufungashaji hadi utumiaji wa mazao yenyewe.   Wakala wa Vipimo ina imani kuwa matumzi ya vipimo sahihi yakizingatiwa  viwanda vingi vitaweza kupata malighafi za kutosha sababu mkulima na mfanyabiashara  kila mtu atakuwa na imani na mwenzake kupitia matumizi ya vipimo sahihi. Msema kweli  na mleta haki katika biashara ni kipimo sahihi  kilichohakikiwa na Wakala wa Vipimo wala siyo vinginevyo.

 Wakala wa Vipimo itaendelea kutoa elimu kwa  wakulima na wafanyabiashara ili wajue thamani ya kuuza kwa kutumia mizani iliyohakikiwa na Wakala wa Vipimo ikiwa ni pamoja na kumsaidia mkulima kupata fedha kulingana na thamani ya mazao yake, kufanya biashara ya haki na kuepusha migogoro/migongano, kukuza uchumi wa mkulima  mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla pamoja na kukuza mauzo ya Pamba ya Tanzania katika soko la Dunia.  Irene alisema kuwa  Wakala wa Vipimo imepewa jukumu la kusimamia usahihi wa vipimo vinavyotumika  au vinavyotarajiwa  kutumika Kisheria  kwenye maeneo  ya biashara  hapa nchini, hivyo  Wakala inaowajibu wa kumlinda  mkulima  wa Pamba  katika uuzaji wa Pamba yake  kwa kutumia vipimo sahihi.
Wakulima wa Pamba wilayani Magu Mkoani Mwanza wakiwasikiliza maafisa wa Wakala wa Vipimo  namna ya kutambua mizani sahihi na ile isiyo sahihi.

Bi. Irene  alisema "elimu kwa pande zote mbili (Mkulima na Mfanyabiashara/Vyama vya Msingi)  ni muhimu lakini zaidi kwa mkulima kwani, mbali ya kutumia muda wake mwingi katika kuandaa shamba, kulima, kupalilia na hata kuvuna bado ameoneka kuwa mnyonge kwenye mazao yake ndiyo maana  kwa sasa tunazunguka Kanda ya Ziwa Mikoa inayolima Pamba   kwa wanunuzi ( vyama vya msingi) na  wakulima kwa ajili ya kutoa elimu  ya matumizi sahihi ya mizani kabla ya uuzaji wa zao la Pamba kuanza.

Bi. Irene alisema kuanzia hatua ya awali ya kuandaa shamba hadi kuvuna mkulima anahitaji matumizi sahihi ya vipimo   lakini wakati wa kuuza mazao, umakini wa  matumizi sahihi ya vipimo unahitajika sana, ambapo kipimo kikiwa sahihi na kikatumiwa kwa usahihi, kitatoa matokeo sahihi kumwezesha muuzaji (mkulima) kupata fedha sawa na thamani ya bidhaa aliyouza.

 Hivyo, nia na lengo la utoaji wa elimu pamoja na  uhakiki mizani  ni kuwasaidia wakulima  kabla ya  msimu wa Pamba  kuanza  wapate elimu ya kutosha hatimaye  mkulima aweze kupata fedha kulingana na thamani ya bidhaa atakayoizalisha na kuwasilisha sokoni. Mkulima naye anao wajibu wa  kumpatia  Afisa Vipimo ushirikiano  kwa kumsaidia  kumpa taarifa  zote atakazo zihitaji, kupeleka mazao yake kwenye chama cha ushirika   au kituo kitakachokuwa kimeteuliwa  na kukubalika na bodi ya Pamba pamoja na  kuhakikisha anauza  Pamba  yake kwa kutumia  mizani sahihi  iliyohakikiwa na Wakala wa Vipimo.

No comments