UFUGAJI WA MBUZI WA NYAMA
Ufugaji wa mbuzi nao umepungua pia huku serikali ikihimiza wananchi kufuga kisasa kwa kuangalia uchumi. Mbuzi wana soko kubwa kila mahali. Hapo ulipo au katika miji mikubwa, lakini si watu wengi wanaofuga mbuzi, tena kibiashara. Kwa hiyo basi, ni vizuri tukajifunza namna nzuri ya kufuga mbuzi wa nyama kisasa. Kama unao tayari, elimu hii itakusaidia kuboresha, lakini kama bado, unaweza kushawishika kuanzisha mradi wa ufugaji mbuzi hata hapo ulipo.
Mbuzi ni tofauti na ng'ombe kwa sababu ni wastahimilivu sana dhidi ya ukame. Wanakula nyasi pia wanakula majani na magome ya miti. Kama nyasi zimekwisha au kukauka wataendelea kuishi na kuzaliana kwa kula majani ya miti.
Kwa ujumla, ufugaji wa mbuzi wa nyama ni fursa muhimu kwa wananchi wengi kujipatia maendeleo hasa ukiongeza thamani kwa kuwafuga kisasa ili kupata soko zuri. Kama utazingatia kanuni za ufugaji, hakika mbuzi anaweza kukupatia faida kubwa na kupunguza umaskini.
Jambo la msingi kabisa ni kwamba lazima uwe na eneo la kufugia, walau shamba lenye ukubwa wa ekari moja. Ni ndani ya shamba hili ambako mbuzi wanatakiwa wajengewe banda bora na wapate eneo la malisho.
Ukiamua kufuga mbuzi kwa lengo la kibiashara unaweza kupata faida kubwa kwa sababu kwa kawaida mbuzi anazaa mara mbili kwa mwaka.
Anabeba mimba kwa miezi mitano (yaani siku 145 hadi 155) na wananyonyesha kwa miezi miwili. Wapo mbuzi ambao wanazaa mapacha, na kwa hiyo unaweza kuongeza kundi lako katika muda mfupi.
Kwa kawaida, mbuzi anakuwa tayari kuzaa anapofikisha miezi 7 hadi 8. Hata kama mbuzi wako siyo wa kuzaa mapacha, lakini kama wanazaa mara mbili kwa mwaka, ukianza na mbuzi 20, una uhakika kwamba kwa mwaka mmoja utakuwa umeongeza mbuzi 40, ambao kwa mwaka unaofuata – ikiwa majike watakuwa 20 kati ya watoto hao, basi utaongeza mbuzi 120 na katika mwaka wa tatu utakuwa umeongeza mbuzi wengine 240, hivyo jumla unaweza kuwa na kundi la mbuzi 320 ndani ya miaka mitatu.
Kama unataka kuzalisha zaidi, basi unaweza kuamua kuwauza madume na kubakiwa na majike ambayo yataendelea kuzaa na kuongeza kundi lako. Faida za mbuzi ni nyingi sana, lakini mbali ya kuwauza wakiwa hai, ukiwachinja utapa nyama, ngozi, kwato na pembe ambazo ni rasilimali nyingine zinazoweza kuuzwa kwenye viwanda ili kuzalisha bidhaa nyingine za ngozi na nta.
Katika nchi nyingi, nyama ya mbuzi inapendwa sana kwa sababu ni tamu na haina lehemu (cholesterol) wala mafuta mengi kulinganisha na nyama nyingine
Post a Comment